SERIKALI imeelezwa kuwa imeamua kutofungua mashtaka dhidi ya vigogo wanaodaiwa kuhusika katika kashfa ya ununuzi wa rada kwa madai kuwa kesi hiyo ingemgusa mmoja wa marais wastaafu, na watu wa karibu wa Rais Jakaya Kikwete, imefahamika.
Taarifa kwamba serikali imekacha kufungua mashitaka kwa lengo la kuwalinda vigogo, mara ya kwanza iliibuliwa na mtandao maarufu wa Wikileaks, ambao umekuwa ukifichua siri nzito katika duru za kiserikali, kidiplomasia na kisiasa katika nchi nyingi duniani. Mchakato wa ununuzi wa rada hiyo iliyouzwa kwa bei ya kuruka ya sh bilioni 40, uliwahusisha watu wa madaraka na kada mbalimbali ambao ni pamoja na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Tony Blair.
Blair anatajwa kuwa ndiye aliyemshawishi aliyekuwa Rais wa Tanzania wakati huo, Benjamin Mkapa, kununua rada hiyo kutoka Kampuni ya kutengeneza silaha ya Uingereza, BAE-Systems wakati aliyekuwa Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa, Clare Short, alikataa katakata, na hata kumshauri Rais Mkapa kwamba Tanzania ni moja kati ya nchi masikini duniani, isingekuwa busara kutumia sh bilioni 40 kununua rada katikati ya umasikini unaonuka.
Mwingine anayetajwa kuishauri vibaya Serikali ni Mbunge wa Bariadi Mashariki, Andrew Chenge (CCM), ambaye kwa muda mrefu amekuwa akitajwa ndani na nje ya chama chake kuhusika na kashfa ya ununuzi wa rada kutoka Kampuni ya BAE- System ya nchini Uingereza.
Chenge, ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Fedha na Uchumi, anatajwa kuhusika kutoa ushauri wa kisheria wakati huo akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ushauri ambao unatajwa kuzingatiwa katika hatua za uamuzi.
Mwingine anayehusishwa na kashfa hiyo ni aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu (BoT), Dkt. Idriss Rashid.
Pamoja na hao, wanatajwa wafanyabiashara wenye asili ya India, lakini ambao wanaishi/walipata kuishi Tanzania, Tanil Somaiya, ambaye alikuwa akimiliki kampuni ya uwakala wa simu ya Shivacom na Sailesh (Shailesh) Vithlani kuwa watu wa kati wa biashara hiyo.
Pamoja na wahusika walioliingiza mkenge taifa kujulikana, Rais Kikwete na Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe kwa nyakati tofauti wametoa msimamo wa serikali.
Rais Kikwete katika mkutano wake na wahariri wa vyombo vya habari, alisema kuwa serikali yake haiwezi kumfikisha mahakamani mtu yeyote kwa vile hakuna rushwa katika ununuzi huo, na badala yake kulikuwa na makosa ya uchapaji katika kuweka kumbukumbu za fedha na mahesabu.
Waziri Chikawe juzi na jana alisema serikali haiwezi kumfikisha mtu yeyote mahakamani katika kesi ya rada, kwani hakuna ushahidi hasa baada ya Serikali ya Uingereza kukataa kuja kutoa ushahidi.
Akijibu swali la Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA) jana bungeni, Chikawe alisisitiza kuwa serikali haina ushahidi wa kumshitaki mtu yeyote mahakamani kwa kashfa ya ununuzi wa rada.
Alisema kutokana na hali hiyo, iwapo kuna mtu yeyote mwenye ushahidi wa kuaminika ndani au nje ya nchi auwasilishe na kwamba wataweza kwenda mahakamani wakati wowote.
“Hili la rada, sina ushahidi, nilisema jana na nasema tena leo ndani ya Bunge hili kama yupo mtu, nje ya Bunge hili mwenye ushahidi ambao ni ‘credible’ wa kumshitaki mtu yeyote ambaye ni Mtanzania, tutamchukua mtu huyo na kwenda naye mahakamani kesho,” alisema Waziri Chikawe.
Katika swali lake la msingi, Mnyika alisema kwa kuwa kampuni ya Uingereza ya silaha za kivita (BAE Systems) ilishakiri makosa ya kutoweka kumbukumbu za fedha na mahesabu katika mchakato wa mauzo ya rada kwa Serikali ya Tanzania, ni dhahiri kuna makosa yalifanyika ya kimanunuzi kati ya pande zote mbili, hali iliyosababisha kuwapo kwa tozo ya pauni milioni 29.5 kama fedha zilizochukuliwa na BAE Systems, hivyo wahusika wachukuliwe hatua.
Pia alihoji serikali imewachukulia hatua gani waliohusika na mchakato wa ununuzi huo kwa upande wa Tanzania.
“Katika hali kama hii tukichukua mtu na kumpeleka tutapata wapi ushahidi na tunaowategemea ni BAE na SFO ambao sasa kule hata kumtaja mtu hauruhusuwi. Na katika ushahidi ni lazima kuwapo na mtoaji na mpokeaji,” alisema.
Wakati serikali ikisema Uingereza imekataa kutoa ushahidi kwa vile hakuna rushwa, Bunge la nchi hiyo hiyo liliwahi kuitaka Serikali ya Tanzania iwafikishe mahakamani wote walioshiriki katika ununuzi wake na kuiingiza nchi katika hasara ya mabilioni ya fedha.
Kupitia kamati yake ya Maendeleo ya Kimataifa, Bunge hilo limesema lingependa kuona watu wote walioshiriki katika mchakato wa ununuzi wa rada hiyo wakifikishwa mahakamani kujibu tuhuma za ufisadi.
Taarifa ya kamati hiyo iliyonukuliwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), ilieleza kwamba wajumbe wake ambao ni wabunge kutoka vyama mbalimbali nchini humo, walisema watatoa ushirikiano wa dhati kwa Tanzania iwapo itaamua kuwashtaki watuhumiwa hao nchini Tanzania au Uingereza.
Kwa mujibu wa BBC, wabunge hao wamesema, mbali na kurudishiwa fedha iliyozidi kwenye ununuzi huo unaosemekana ulitawaliwa na rushwa, Serikali ya Tanzania inapaswa kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wote haraka iwezekanavyo ili haki itendeke.
Namna walivyochota mamilioni
Kwa mujibu wa rasimu ya ripoti ya SFO (Taasisi ya Uchunguzi Makosa ya Jinai ya Uingereza), Chenge alipokea malipo ya jumla ya dola za Marekani milioni 1.5 (zaidi ya sh bilioni 1.5) kati ya Juni 1997 na Aprili 1998 kutoka Benki ya Barclays, tawi la Frankfurt.
Fedha hizo zililipwa katika benki ya Barclays huko Jersey – Uingereza, katika akaunti inayomilikiwa na kampuni iliyotajwa kwa jina la Franton Investment Limited. Kampuni hiyo imetajwa kumilikiwa na Chenge, ikiwa ni maalumu kwa ajili ya uhamishaji fedha kiasi cha dola za Marekani 600,000 (zaidi ya sh milioni 600).
Dola hizo 600,000 za Marekani zilihamishwa kutoka kwenye akaunti ya kampuni ya Chenge kwenda kwenye akaunti nyingine, inayomilikiwa na Kampuni ya Langley Investments Ltd, iliyokuwa ikiendeshwa na Dkt. Idriss (aliyewahi pia kuwa Mkurugenzi wa TANESCO).
Septemba 20, mwaka 1999, Chenge binafsi aliidhinisha uhamishaji wa dola za Marekani milioni 1.2 (zaidi ya sh bilioni 1.2) kutoka akaunti ya Kampuni (yake) ya Franton kwenda Royal Bank of Scotland International, huko Jersey.
Source: Tanzania daima
Follow me on Twitter @Nyamtee or Facebook @leilamaingu for more news, entertainment, celeb gossip and more....
No comments:
Post a Comment