Saturday, 14 July 2012

Wema Sepetu Avamiwa na Majambazi


Na Musa Mateja:
SIKU chache baada ya kuanika utajiri wake, staa wa Bongo Movies, Wema Isaac Sepetu (pichani), amevamiwa na majambazi na kukombewa vitu kadhaa huku gari lake aina ya Toyota Lexus lenye namba za ujsali T 211 BXR likinusurika kuibwa, Ijumaa lina kila sababu ya kukujuza.
Tukio hilo lilijiri usiku wa kuamkia Julai 9, mwaka huu, nyumbani kwake Kijitonyama, jijini Dar es Salaam ambapo majambazi hayo yaliingia ndani kwake kwa kuruka ukuta licha ya kwamba kuna walinzi wawili.

KIKWAZO CHA NGUVU
Hata hivyo, baada ya kuzamia ndani ya geti, majambazi hayo yalishindwa kuingia ndani kabisa kutokana na milango madhubuti iliyopo kwenye nyumba hiyo ya kisasa.

WAJIPOZA KIDOGO
Kule ndani ya geti, walivunja mlango wa gari hilo na kuiba vitu mbalimbali kama kifaa cha kudhibiti mwenendo wa umeme ndani ya gari (control box), vifaa vya kufungulia vioo, milango na madirisha (power window) na vioo vinavyomuongoza dereva kuona nyuma (side miller).
Vitu vingine ambavyo viliambatana na wizi huo ni ‘makapeti’ ya ndani na vitu vingine vidogovidogo ambavyo vilikuwa ndani ya geti hilo.

WEMA AWASHANGAA WALINZI WAKE
Akielezea mazingira ya tukio hilo, Wema alisema kuwa hata yeye ameshangazwa na uvamizi huo ambao umemfanya kuibua maswali mengi kuliko majibu hasa akizingatia kuwa tukio hilo limetokea wakati nyumba yake ina walinzi wawili.
“Ni kweli nimeibiwa hivyo vitu kwenye gari na vingine vilikuwa nje, ila mazingira ya kuvamiwa na yale majambazi yananitia shaka sana maana walinzi wangu wawili walikuwepo muda wote, sasa sijui nini kilitokea?” alisema Wema kwa sauti ya kupooza.
Akaendelea: “Sikuwa na namna kwao, nilikwenda kutoa taarifa katika Kituo cha Polisi Oysterbay ili angalau nisaidiwe utatuzi wa jambo hili sambamba na kuwabananisha walinzi wangu ambao walikuwepo usiku wa tukio.
“Naamini kama geti la kutokea nje lingekuwa legelege, wangeiba na gari lenyewe. Lakini hili geti ni gumu, mpaka kulifanya lifunguke wangeweza kuchukua masaa matano ambapo kungekuwa kumekucha.”

INAWEZEKANA SABABU IKAWA HII?
Katikati ya Juni mwaka huu, staa huyo ambaye pia ni Miss Tanzania 2006, alitangaza kupitia runinga kwamba anamiliki nyumba hiyo huku akisema ina kila kitu ndani.
Kwa mujibu wa picha zilizoenea kwenye mitandao mbalimbali Bongo, sebule ya nyumba hiyo inaweza kushawishi ‘wazee wa kazi’ kunyatia kwani Meneja wa Wema, Martin Kadinda alisema manunuzi ya nyumba hiyo pamoja na samani zake shilingi Milioni 4OO ‘ziliteketea’.

HABARI ZA KIPOLISI ZATHIBITISHA
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi, Kinondoni, Charles Kenyera hakupatikana siku ya Jumanne kuzungumzia tukio hilo licha ya kwamba, habari za kipolisi zilithibitisha Wema kukumbwa na uvamizi wa watu wanaodhaniwa ni majambazi.

Source:globalpublishers,habarimoto

No comments:

Post a Comment