Wednesday, 28 August 2013

KAGAME HATAKANYAGA TENA ARDHI YA TANZANIA.....WABUNGE WA RWANDA WASUSA JIJINI ARUSHA...



RAIS Paul Kagame wa Rwanda, sasa hayupo tayari kukanyaga ardhi ya Tanzania kutokana na kile kinachoonekana kuwa ni mgogoro wa kidiplomasia unaoendelea kati yake na Rais Jakaya Kikwete.

Wakati hayo yakifikia hapo, kikao cha Bunge la Afrika Mashariki (EALA), linakoketi mjini Arusha kilivunjika baada ya Spika wa bunge hilo, Magreth Zziwa, kugongana kauli na Mbunge mmoja wa Rwanda jambo lililosababisha wabunge wote wa Rwanda kususia kikao na kutoka nje ya ukumbi wa Bunge.

Mwenendo wa hayo yaliyojitokeza jana katika Bunge la Afrika Mashariki hadi kikao kuvunjika, msingi wake ni mgogoro unaowagusa wakuu hao wawili wa dola.

Habari zilizolifikia gazeti hili toka katika vyanzo vyake mbalimbali vilivyo ndani na nje ya mipaka ya Tanzania, lakini pia katika vikao vya Bunge hilo la Afrika Mashariki vinavyoendelea jijini Arusha zinaeleza kuwa, Rais Kagame hata kama ataalikwa kuja nchini leo, hatakuja.

MTANZANIA Jumatano limedokezwa kuwa jambo hilo tayari limethibitishwa na Wabunge wa Rwanda wanaohudhuria vikao vya (EALA).

Taarifa toka ndani ya Bunge hilo zilizolifikia MTANZANIA Jumatano zinaeleza kuwa, tayari mzimu wa msigano huo uliojitokeza baina ya wakuu hao wawili wa dola, umeanza kuwavuruga wabunge hao baada ya jana kikao cha Bunge hilo kuvunjika, kutokana na kuibuliwa kwa hoja ya kutaka vikao vya Bunge hilo kufanyika kwa utaratibu wa kuzunguka kila nchi.

Zinaeleza zaidi kuwa; Ni katika hoja hiyo wabunge wa Kenya na Rwanda walionekana kuungana na kuwa kitu kimoja na hivyo kususia kikao hicho cha jana, jambo ambalo lilimlazimisha Spika wa Bunge hilo, Magreth Zziwa kuvunja kikao.



HALI ILIVYOKUWA 

MTANZANIA Jumatano limedokezwa kuwa, wabunge hao walianza kutoka ndani ya kikao kilichokuwa kikiendelea jana, baada ya mmoja wa wabunge hao kutoka Rwanda, James Ndahiro kuomba mwongozo kwa Spika.

Habari zinaeleza kuwa chanzo cha mbunge huyo wa Rwanda kuomba mwongozo, kilitokana na Mbunge kutoka Kenya, Peter Mathuki kutoa hoja ya kutaka suala la vikao hivyo kufanyika kila nchi wanachama, lijadiliwe.

“Sasa baada ya mbunge huyo wa Kenya kutaka suala la vikao vya Bunge kufanyika kila nchi wanachama yaani ‘rotation’ lijadiliwe pale kikaoni, Spika akamwambia hilo ni jambo la haraka sana na ikizingatiwa imebaki wiki moja vikao viishe na kwamba kama anataka lizungumziwe, alilete kama ‘motion’.

“Baada ya Spika kujibu hivyo, ndipo mbunge wa Rwanda akaomba mwongozo kwa Spika…Spika akamjibu kwamba anataka mwongozo gani tena wakati ameshamjibu yule wa Kenya, ndipo wabunge wa Rwanda wakatoka ndani ya kikao wakisema hawataki kuburuzwa huku wakifuatiwa na wa Kenya.”

Taarifa zaidi zilieleza kuwa kitendo hicho ambacho kilisababisha kikao kuvunjika, kilikwamisha kuapishwa kwa Waziri mpya wa EALA kutoka Rwanda.

Ilielezwa kuwa baada ya wabunge hao kutoka, Spika aliahirisha kikao kwa kutumia kanuni kwamba, baada ya dakika 15 warudi.

“Baada ya dakika 15 tuliporudi, wabunge wakawa wachache huku wale wa Rwanda na Kenya hawakurudi tena na waliorudi walikuwa jumla 13 pamoja na Spika kati ya wabunge 45. Ndipo Spika akasema hatuwezi kuendelea na kikao kutokana na uchache wa wabunge, hivyo kikaahirishwa hadi kesho (leo),” kilisema chanzo chetu hicho.

Hata hivyo wakati hayo yanajitokeza, utaratibu wa vikao vya Bunge la Afrika Mashariki  unaelekeza kuwa vitafanyikia Arusha ambako ni makao makuu.

Habari zilizolifikia gazeti hili zinaeleza kuwa, Kamati ya kuratibu Mambo ya Bunge iliyokutana Entebe Uganda, ilipanga kuwa kwa mwaka vikao vya Bunge vitakuwa sita huku vitatu vikifanyika Arusha ambako ni makao makuu, kimoja Nairobi na vingine viwili bado haijajulikana.

Pamoja na Kamati kufikia uamuzi huo, bado inaelezwa kuwa baadhi ya wabunge wanapinga vikao hivyo kuendelea kufanyika na hasa wa Rwanda ambao inadaiwa kuwa wamepewa maagizo fulani kutoka kwenye Serikali yao

Mbali na hilo la vikao, nyufa nyingine zinazoelezwa kuhatarisha msingi wa Bunge hilo, ni kile kinachodaiwa kuwapo kwa utendaji wa upendeleo wa Spika, Margaret Zziwa.

Kwamba Spika Zziwa amekuwa akishutumiwa kupanga safari za nje kwa upendeleo na kwamba hazieleweki zinapangwaje.

KAGAME KUTOKANYAGA TANZANIA

Wakati hayo yakijiri, imeelezwa kuwa hata Rais Kagame, akialikwa kuhutubia vikao vya Bunge hilo, hataweza kuja nchini kutokana na mgogoro uliopo.

Taarifa zilizolifikia gazeti hili toka ndani ya bunge la EALA, zinaeleza kuwa wabunge kutoka Rwanda wananung’unika vikao kufanyika Arusha na wameeleza bayana kwamba itakuwa vigumu kwa rais wao kuja hapa nchini endapo ataalikwa na Spika wa Bunge hilo kuja kuhutubia katika vikao hivyo.

“Kwa kawaida vikao vya bunge vinapofanyika, mara nyingi anayehutubia vikao ni Mwenyekiti wa EAC, ambaye kwa sasa ni Yoweri Museveni na rais wa nchi ambako vikao vinafanyika, lakini wakati mwingine spika anaweza akaamua na kumteua rais kutoka nchi yoyote.

“Sasa Spika akimteua Kagame ni dhahiri itakuwa ngumu kuja Tanzania kutokana na mgogoro unaoendelea baina yake na Rais Kikwete,” kilisema chanzo chetu hicho cha habari.

Msigano wa kauli baina ya viongozi hao wakuu wa dola, ulijitokeza baada ya Rais Kikwete kutoa ushauri kwa Rais Kagame wa kukaa meza moja na waasi wa FDLR.

Hata hivyo baada ya siku chache, Kagame alinukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari nchini Rwanda akimkejeli Kikwete hadi kufikia kutoa kauli zenye vitisho dhidi yake.

Tangu Rais Kikwete alipotoa ushauri huo, Kagame amekuwa akiendelea kutoa lugha zisizo na staha kwa Tanzania.

Baadhi ya vyombo vya habari nchini Rwanda, navyo vimekuwa na mwelekeo huo huo, ambapo hivi karibuni vilianza kuhusisha ushauri huo wa Rais Kikwete kuwa msingi wake unatokana na undugu uliopo kati ya mke wake, Mama Salma Kikwete na wabaya wa Kagame.

Kwamba mke wa Rais Kikwete ni binamu wa kiongozi wa zamani wa Rwanda, Juvenal Habyarimana, habari ambazo zimekanushwa vikali na Serikali.

Ni katika mwenendo huo huo, wiki iliyopita ilibainika kuwa Rwanda na Uganda zinakusudia kutangaza kujitoa kutumia Bandari ya Dar es Salaam kuanzia mwezi ujao.

Katika hilo, leo Marais Uhuru Kenyatta wa Kenya, Yoweri Museveni wa Uganda pamoja na Paul Kagame wa Rwanda, wanatarajiwa kuzindua Gati ya bandari ya Mombasa yenye thamani ya dola za Marekani milioni 66.7 ambayo ni zaidi ya Sh bilioni 100 za Kitanzania.

Bandari hiyo ambayo itaongeza uwezo kwa asilimia 33, Rais Museveni ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya Afrika Mashariki (EAC), ataongoza zoezi hilo la uzinduzi.

Baadhi ya wachambuzi wa sayansi ya kiuchumi, wanasema kuwa endapo Rwanda na Uganda zitajitoa kutumia bandari ya Dar es Salaam, hizo zitakuwa ni habari mbaya kwa nchi.



Credit -Mtanzania

Follow me on Facebook @leilamaingu for news, fashion, entertainment, celeb gossip and more.....

No comments:

Post a Comment